Aina za MashairiZifuatazo ni aina za mashairi kulingana

Aina za Mashairi

Zifuatazo ni aina za mashairi kulingana na idadi ya mishororo katika kila ubeti

AINA

#MISHORORO

MFANO

Umoja/tathmina

1

 

Tathnia

2

 

Tathlitha

3

 

Tarbia

4

 

Takhmisa

5

 

Tasdisa

6

 

Usaba

7

 

Ukumi

10

 

Tanbihi: Aina za Mashairi ni tofauti na Bahari za Ushairi. Aina za mashairi huzingatia idadi ya mishororo katika kila ubeti ilhali Bahari za Shairi hutegemea na muundo wa shairi kwa kuzingatia vina, mizani, vipande na mpangilio wa maneno. Shairi moja haliwezi kuwa la aina mbili (k.v tarbia na takhmisa) lakini shairi linaweza kuwa katika bahari zaidi ya moja.

Bahari za Ushairi


 Ushairi • Bahari za Ushairi


Bahari za ushairi ni nyingi sana. Shairi huainishwa katika bahari fulani kulingana na mtindo wake, umbo lake na matumizi ya lugha.

Baadhi ya bahari za ushairi ni:

  1. Utenzi – shairi ndefu lenye kipande kimoja katika kila mshororo.
  2. Mathnawi – ni shairi la vipande viwili (ukwapi na utao) katika kila mshororo.

Ewe mtunga silabi, na sauti ya kinubi,
Majukumu hatubebi, maadamu hatushibi,
Mateso kwa ajinabi, kwa mabwana na mabibi
Ukija hayatukabi, karibia karibia

  1. Ukawafi – ni shairi la vipande vitatu (ukwapi, utao na mwandamo) katika kila mshororo.

Nashindwa nikupe nini, nishukuru kwa malezi, mapenzi na riziki,
Ni pendo kiasi gani, lishindalo la mzazi, kweli mama hulipiki,
Ulinilinda tumboni, ukilemewa na kazi, ila moyo huvunjiki,
Kanilisha utotoni, mavazi pia malazi, ukitafuta kwa dhiki.

  1. Mavue – Shairi la vipande vinne (ukwapi, utao, mwandamo na ukingo) katika kila mshororo.

Sisi walipa ushuru, wajenga taifa, tena kwa bidii, twahangaishwa,
Tumenyimwa uhuru, tuna mbaya sifa, hatujivunii, tunapopotoshwa,
Kila tunapopazuru, damu na maafa, hatutulii, hali ya kutishwa

  1. Ukaraguni – shairi ambalo vina vyake vya kati na vya mwisho hubadilika kutoka ubetio mmoja hadi mwingine.

Vina Ubeti 1: —ni, —mi,
ubeti 2: —ta, —lo,
ubeti 3: —po, —wa,

  1. Ukara – shairi ambalo vina vya kipande kimoja havibadiliki kutoka ubeti mmoja hadi mwingine, lakini vina vya kipande kingine hubadilika. Kwa mfano, vina vya kati vinafanana kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho lakini vina vya kipande cha mwisho vinabadilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.

vina Ubeti 1: —shi, —ma,
ubeti 2: —shi, —ko,
ubeti 3: —shi, —le,
ubeti 4: —shi, —pa

  1. Mtiririko – shairi ambalo vina vyake vya mwisho na vya kati havibadiliki kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho.

kwa mfano vina vikiwa ( —ni, —ka) kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho.

  1. Mkufu/pindu – Shairi ambalo neno la mwisho au kifungu cha mwisho cha maneno katika ubeti mmoja, hutangulia katika ubeti unaofuatia.

Hakika tumeteleza, na njia tumepoteza,
Nani wa kutuongoza, aliyepewa uweza,
Filimbi akipuliza, tusiyeweza kupuuza,
Bali twaisikiliza, bila ya kuzungumza,

Bila ya kuzungumza, wala mwendo kulegeza,
Tumwandame ja mwangaza, kututoa palipo giza,
Penye dhiki ya kuliza, bila sauti kupaza
Pengo hili kulijaza, ni nani anayeweza,

  1. Kikwamba – Neno moja au kifungu cha maneno hurudiwarudiwa kutanguliza mishororo au ubeti katika shairi.

Jiwe hili lala nini, ila moshi na majani,
Jiwe linalala lini, litokapo vileoni,
Jiwe hili halineni, lina macho halioni,
Jiwe na tulibebeni, tulitupe mitaroni

  1. Kikai – Shairi lenye kipande kimoja kifupi (chenye mizani chache kuliko kingine) Mfano (8,4)

Nani binadamu yule, adumuye,
Anayeishi milele, maishaye
Jenezani asilale, aluliye,
Kaburi liko mbele, sikimbiye.

  1. Msuko – Shairi ambalo kibwagizo/mshororo wa mwisho ni mfupi kuliko mishororo mingineyo. K.v (8,8) (8,8) (8,8) (8).

Hawajazawa warembo, usidhani umefika,
Ukisifiwa mapambo, jinsi ulivyoumbika,
Akipata jipya umbo, ‘tabaki kihangaika,
Usidhani umefika.

  1. Mandhuma – shairi ambalo kipande kimoja hutoa hoja, wazo ama swali, huku cha pili kikitoa jibu/suluhisho.
  2. Malumbano – Mashairi mawili ambapo mshairi mmoja hutunga shairi akijibu au kupinga utunzi wa mshairi mwengine.
  3. Ngonjera – Shairi lenye wahusika wawili wanaojibizana. K.m. Ubeti wa kwanza, mwalimu, na wa pili, mwanafunzi.
  4. Sakarani – Shairi lenye bahari zaidi ya moja.
  5. Sabilia – Shairi lisilokuwa na kibwagizo. Kituo (mshororo wa mwisho) hubadilika kutoka ubeti hadi ubeti.
  6. Shairi huru – shairi lisilozingatia sheria za ushairi
  7. Shairi guni – shairi lenye makosa ya arudhi za shairi

Uchambuzi wa Mashairi


FasihiUshairi • Uchambuzi wa Mashairi


Yafuatayo ni mambo muhimu unayohitajika kuzingatia kila unapochambua shairi.

  1. Muundo/Umbo la shairi
  2. Uhuru wa Mshairi
  3. Maudhui
  4. Dhamira
  5. Mtindo wa / Mbinu za Lugha

1.      Muundo/Umbo la Ushairi

Katika umbo wa shairi, tunaangazia jinsi shairi lilivyoundwa kwa kuangazia mizani, vina, mishororo n.k Aidha, ni muhimu kutaja aina na bahari za shairi zinazohusiana na kila sifa uliyoitaja.

    1. Idadi ya mishororo katika kila ubeti – Tumia idadi ya mishororo kubainisha aina ya shairi hilo.
      Kwa mfano: Shairi lina mishororo minne katika kile ubeti, kwa hivyo ni Tarbia
    2. Idadi ya mizani katika kila mshororo na katika kila kipande cha mshororo.
      Kwa mfano: Kila mshororo una mizani kumi na sita: nane katika utao na nane katika ukwapi.
    3. Idadi ya vipande katika kila mshororo – Taja ikiwa shairi lina kipande kimoja, viwili, vitatu au vinne kisha utaje bahari yake.
    4. Kituo, kiishio au kibwagizo – Ikiwa mstari wa mwisho umerudiwa rudiwa, basi shairi lina kibwagizo au kiitikio, la sivyo lina kiishio.
    5. Vina – Zingatia vina vya kati na vya mwisho kutoka ubeti mmoja hadi mwingine. Kisha utaje ikiwa ni Mtiririko, Ukara au Ukaraguni

2.      Uhuru wa Mshairi

Mshairi hafungwi na kanuni za kisarufi za lugha katika utunzi wa shairi. Anaweza kufanya makosa ya kisarufi kimakusudi ili shairi lizingatie umbo fulani. Zifuatazo ni njia mbalimbali ambazo mtunzi wa shairi anaweza kutumia kuonyesha uhuru wake.

    1. Inkisari – kupunguza idadi ya silabi katika neno ili kusawazisha idadi ya mizani katika mshororo.
      mfano: kubadilisha ‘nimeona aliyenipenda‘ kuwa ‘meona alenipenda‘.
    2. Mazda – kuongeza silabi katika neno ili kusawazisha idadi ya mizani katika mshororo.
      mfano: afya ukijaliwa kuwa afiya ukijaliwa .
    3. Tabdila – kubadilisha silabi ya mwisho ili kustawazisha urari wa vina katika kipande bila kuathiri mizani.
      mfano: yahuzunisha dunia kuwa yahuzunisha duniya .
    4. Kuboronga Sarufi -ni mbinu ya kupangua mpangilio wa maneno ili kuleta urari wa vina au mdundo wa ushairi.
      mfano: siku hiyo ikifika kuwa ikifika hiyo siku .
    5. Utohozi – Kuswahilisha Maneno – Wakati mwingine mshairi anaweza kubadilisha neno la lugha nyingine litamkike kwa Kiswahili ili kudumisha mdundo wa kishairi na pia kupata neno mwafaka litakalotimiza arudhi za kiushairi.
      mfano: tukapata intaneti badala ya tukapata ‘internet’ ama mtandao wa tarakilishi.

3.      Maudhui

Maudhui ni jumla ya ujumbe na mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika shairi fulani. Haya ni mambo yanayotajwa katika hadithi na yanaweza kujumuisha mawazo zaidi ya moja. Maudhui husaidia kujenga dhamira ya shairi.

4.      Dhamira

Dhamira ni lengo, dhumuni au nia ya mtunzi wa shairi. Mtunzi wa shairi anaweza kuwa na kusudi la kutuonya, kututahadharisha au kutunasihi kuhusiana na jambo fulani.

5.      Mtindo wa Lugha

Mtindo wa lugha hurejelea namna mbalimbali ambazo mshairi anatumia mbinu za lugha. Mshairi anaweza kutumia mbinu za lugha. kama vile: Tanakali za Sauti, Istiara, Takriri, Semi n.k

 

One thought on “Aina za MashairiZifuatazo ni aina za mashairi kulingana

Leave a comment